Thursday, 3 November 2011

                  CORONATION DAY                        



 JUMUIYA ya Rastafari nchini Tanzania (Taramo) imeandaa tamasha maalumu la kumbukumbu ya kutawazwa kwa mfalme Haile Selassie maarufu kama 'Coronation day' inayoadhimishwa kila Novemba tano kwa kufanya mkusanyiko wa burudani wa muziki 
wa asili ya reggae. 


Mwenyekiti wa Taramo, Ras Bumijah alisema, tamasha hilo lisilo la kiingilio limepangwa kufanyika kesho ukumbi wa Kilimanjaro 2000, Mwenge jijini Dar es Salaam na litaambatana na muziki wa bendi na wanamuziki wa miondoko ya reggae. 


Alizitaja bendi na wanamuziki wa miondoko hiyo watakaotumbuiza ni Jhikoman, Ras Gwandumi na Machifu Band, Roots Rockers, Ras Mizizi, Ras Kabonga na muziki wa asili ya kiafrika na kuongeza kuwa tamasha litaanza saa 12 jioni. 


Alisema kufanyika kwa tamasha hilo ni mwendelezo wa kuenzi utawazo wa mfalme Haile Selassie na kushuhudiwa na mataifa zaidi ya 72 duniani. 


Alisema katika kuenzi siku hiyo, marastafari nchini walianza maadhimisho hayo Novemba 2 mwaka huu kwa mkusanyiko uliofanyika Kigamboni ambapo pamoja na mambo mengine ulihusisha shughuli za kijamii za kusafisha fukwe na burudani ya muziki wa asili ya reggae na kesho ndiyo siku ya hitimisho ya kumbukumbu hiyo. 


"Hii ni siku muhimu kwa jumuiya ya Rastafari kote duniani, hukusanyika kwa ajili ya kukumbuka utawazo wa mfalme Haile Selassie ambaye kwa mujibu wa maandiko Haile ni 
kizazi cha ukoo wa mfalme Suleiman. 


Ni tamasha linalojumisha wanajamii ya imani ya Rastafari na wapenzi wa burudani wa muziki wa reggae kwani ni siku ya amani na upendo kwa kila mtu milele," alisema Ras Bumijah. 


Aliongeza kuwa, tamasha hilo litahusisha pia maonesho ya mavazi ya asili ya jamii ya Rastafari na mitindo ya mavazi yanayozingatia mila na desturi ya kiafrika kwa kuamini kuwa 
Haile Selassie ambaye alikuwa mfalme wa Ethiopia ni mmoja wa viongozi muhimu barani Afrika wanaopaswa kuendelea kukumbukwa.

No comments:

Post a Comment