Serikali yakubali kulipa 94 bilioni Dowans |
![]() SERIKALI imeamua kuilipa kampuni ya Dowans Tanzania Ltd, Sh 94 bilioni kama ilivyoamuliwa na Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi (ICC) na kuwataja wamiliki na wakurugenzi wa kampuni hiyo ambao wote si Watanzania. Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja alisema hayo jana jijini Dar es Salaam, katika mkutano wake na waandishi wa habari. Alisema Sh.185 bilioni zilizokuwa zikitajwa kwenye vyombo vya habari ndizo ambazo kampuni ya Dowans iliiomba ICC ilipwe fidia kwa Tanesco kwa kukatiza mkataba walioingia wa kufua umeme, lakini mahakama iliafiki ilipe dola 65 milioni za Marekani. Alisema fedha hizo zitalipwa baada ya pande hizo zitasajili uamuzi huo katika mahakama kuu. “ Serikali tumekwishaamua kuwa tutailipa Dowans dola za Marekani 65 milioni, kama ilivyoamuliwa na ICC ambazo ni sawa na Sh 94 bilioni, kuchelewa kuwalipa kutatufanya tulipe riba ya asilimia 7.5,” alisema. “ Siyo kwamba kiasi tunachotakiwa kulipa ni kidogo, ila tumeona ni muhimu Watanzania wakafahamu kiasi halisi ambacho tunatakiwa kuilipa Dowans,” alisema. Alisema wameamua kulipa baada ya mwanasheria mkuu wa serikali, kusema kuwa hukumu hiyo ilikuwa halali na kuipinga kungeizidishia serikali gharama. “Mwanasheria mkuu wa serikali ameshauri kutekeleza uamuzi wa mahakama ya usuluhishi endapo uamuzi huo utasajiliwa katika mahakama kuu ya Tanzania,” alisema Ngeleja. Aidha Ngeleja aliwataja wamiliki wa Dowans Tanzania Ltd, na hisa wanazomiliki katika mabano kuwa ni Dowans Holding S.A ya Costa Rica (81) na Portek Systems and Equipment (PTE) LTd (54). Aidha Waziri Ngeleja huku akirejea barua ya Wakala wa Usajili wa Kampuni (Brella), aliwataja wakurugenzi na nchi wanazotoka kuwa ni Andrew James Tice (Canada) na Gopalakrishnan Balachandaran (India). Wakurugenzi wengine kwa mujibu wa Waziri Ngeleja ni Hon Sung Woo (Singapore), Guy Picard (Canada), Sulaiman Al Adawi (Oman) na Stanley Munai (Kenya). Kiini cha sakata hilo kilianza mwaka 2006, wakati Tanesco ilipoingia mkataba wa mauziano ya umeme wa Tanesco na kampuni ya Richmond Developmen LLC. Miezi sita baadaye mkataba huo ulihamishiwa kwa kampuni ya Dowans Holdings ya nchini Costa Rica na baadaye kwa Dowans Tanzania Ltd, Wakati wa utekelezaji wa mkataba huo, ilizuka hoja kutoka kwa watu mbalimbali wakiwemo wabunge kwamba mkataba baina ya Tanesco na Richmond haukuwa halali kisheria hivyo usingeweza kurithiwa na Dowans. Suala hilo lilizua mjadala mkubwa hali ambayo Tanesco kwa kuwatumia mawakili wa kampuni ya Rex Attorneys ya jijini Dar es Salaam walivunja mkataba huo. Baada ya kuvunjwa kwa mkataba huo, ndipo kampuni hiyo ikalipeleka suala hilo ICC kama walivyokubaliana na Tanesco kwenye mkataba. Uamuzi huo wa ICC ulizua mjadala katika siku za hivi karibuni baada ya viongozi wa serikali kutofautiana kuhusu kuilipa kampuni hiyo au kutoilipa. Wakati Waziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Samwel Sitta, akiitaka serikali kutolipa Dowans kwa kuwa kufanya hivyo ni uhujumu wa nchi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Frederick Werema akitaka kampuni hiyo ilipwe. |
No comments:
Post a Comment